Real Madrid yatwaa ubingwa wa Uefa Champions League 2017/18

Klabu ya Soka ya Real Madrid imefanikiwa kutwaa Kombe la UEFA Champions League, kwa mara ya 3 mfululizo baada ya kuicharaza Liverpool goli 3-1

Madrid

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane anakuwa kocha wa kwanza kushinda kombe hilo mara tatu mfulizo huku Mchezaji Gareth Bale akiwa mchezaji wa kwanza kutoka benchi na kufunga magoli mawili.

Kwenye fainali hiyo kama kuna mtu alikuwa na usiku mbaya, basi ni kipa wa Majogoo wa Anfield, Loris Karius, ambaye alitoa zawadi ya bao la kwanza, lililofungwa na Karim Benzema na lile la tatu, ambalo alijaribu kudaka shuti la Bale, ambalo lilipigwa kisawasawa.

Liverpool wao walipata bao lao la kujifariji kupitia kwa Sadio Mane, lakini kwa fainali hiyo ya usiku wa jana, mabao yote yalipigwa kipindi cha pili, huku Real Madrid wakiweka rekodi ya kubeba ubingwa wa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo, huku ikiwa mara yao ya 13 katika historia.

Ilikuwa fainali ya wanaume na wavulana baada ya kuonekana wazi kabisa, Liverpool ilikosa uzoefu mbele ya wapinzani wao, ambao karibu mastaa wake wote walikuwa wamecheza mechi zaidi ya moja za fainali ya michuano hiyo ya Ulaya.

Hali mbaya kwa Liverpool ilianzia pale supastaa wao, Mohamed Salah alipoumia bega kwenye kipindi cha kwanza baada ya kupigana vikumbo na Sergio Ramos na baada ya tukio hilo, kila kitu kilibadilika na Los Blancos walianza kutawala mchezo, huku mabeki wa kocha Zinedine Zidane wakicheza kwa kujiachia kabisa.

Ukweli ni kwamba haikuwa mechi ngumu kwa Real Madrid, wakimiliki mpira kwa asilimia 61, huku mashuti yao sita yakilenga goli, wakati Liverpool walipiga mashuti mawili tu.

Kwenye mechi hiyo, wachezaji wawili waligongesha mwamba, Isco kwa upande wa Real Madrid na Mane kwa vijana wa Jurgen Klopp, ambaye kabla ya mechi hiyo alidai kwamba, hawezi kuwakubali Madrid kama ni timu bora kwa sababu walikuwa bado hawajacheza na timu yake ya Liverpool.

Lakini, nadhani kwa sasa akiulizwa swali la kuhusu ubora wa Madrid, atakuwa na majibu yaliyosahihi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s