Mourinho ndani ya hesabu kali za kuandaa jeshi la msimu ujao Man Utd

Guardiola na jeshi lake la Manchester City wanaendeleza kula bata baada ya juzi Jumapili kukabidhiwa kombe lao la Ligi Kuu England, lakini huko kwa mpinzani wake, Jose Mourinho hakuna kulala kabisa.

jose-pep-1

Mourinho na mabosi wa Man United wameanza kupambana kusaka dawa ya kumzima Guardiola, imeelezwa, ambapo harakati za kuingia na kutoka sambamba na vikao zimeshika kasi pale Old Trafford. Msimu huu Mourinho amekuwa mnyonge mbele ya Guardiola ambaye kikosi chake kimeuwasha moto kwelikweli na kutangaza ubingwa mapema kwa tofauti ya pointi 13 huku akiwa amepoteza michezo miwili tu.

Katika michezo hiyo aliyopoteza Guardiola mmoja amechapwa na Liverpool kwa mabao 4-3 kisha akachapwa na Man United mabao 3-2, ambapo kama Man United ingepoteza mchezo huo basi City ingetangaza ubingwa wake mbele ya United tena ndani ya Old Trafford.

Hata hivyo, Mourinho aliwaonya wachezaji wake mapema kuwa jeshi lake haliwezi kugeuzwa daraja la mahasimu wao kutangazia ubingwa na jeshi la Guardiola likafa tena kibabe kwelikweli.

Kwa mujibu wa mtandao wa 90min.com, ishu kubwa inayoendelea Old Trafford kwa sasa ni usajili wa mastaa wa nguvu barani Ulaya, ambapo Mourinho na Mtendaji Mkuu wa Manchester United, Ed Woodward wamejifungia na kutengeneza orodha moja matata ya mastaa ambao watakwenda kuvaa jezi za United msimu ujao.

Jose anataka kujenga kikosi matata kitakachotoa ushindani mbele ya vigogo wengine barani Ulaya kama Barcelona, Real Madrid, Bayern Munich, PSG na Manchester City ambayo imekuwa ikiwasumbua tangu ilipoanza kunolewa na Guardiola.

Mourinho

Orodha ya mastaa hao kama Mourinho atafanikiwa kuwanasa wote basi ni tishio kubwa kama tetemeko na kamwe usiombe ukakutana nayo uwanjani ni lazima bao za kutosha zitakuhusu.

Jina la kwanza kuchomoza kwenye orodha ya mastaa wapya ambao Mourinho anawataka kwa ajili ya kutengeneza jeshi lake la msimu ujao lipo la supastaa wa Brazil, Neymar ambaye mipango iliyopo ni kumfanya kuwa mshambuliaji wa kati atakayekuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza.

Kwa muda mrefu sasa, Man United imekuwa ikihusishwa na Neymar, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji ghali duniani baada ya kununuliwa na matajiri wa Paris, PSG akitokea Barcelona ya Hispania.

Usajili wa Neymar ulikuwa gumzo kwelikweli, ambapo PSG ililipa Pauni 198 milioni tena keshi kwa Barcelona na katika msimu wa kwanza tu, Mrazili huyo ameiwezesha kushinda taji la Ufaransa kabla ya kuumia na sasa yupo nje akiuguza majeraha.

Hata hivyo, kama dili hilo la kumnasa Neymar litajibu basi Man United watalazimika kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu England bila huduma ya kiungo wake fundi, Paul Pogba.

Iko hivi, PSG imekuwa ikijaribu kutaka kumsajili Pogba kutoka Old Trafford na taarifa zinasema kwamba, Man United wanaweza kuwa tayari kumhusisha kwenye dili la Neymar ambako, watatakiwa kuilipa PSG dau la Pauni 200 milioni pamoja na Pogba.

Habari zinaeleza kuwa, kwa Mourinho kumuachia mchezaji hata awe staa mkubwa kiasi gani halijawahi kuwa tatizo kabisa kwani, pengo linaweza kuzibwa na mastaa watatu ambao wako tayari kutua Old Trafford wakati wowote.

Katika mastaa hao kuna kiungo wa nguvu wa Stoke City ambayo imeshuka daraja, Xherdan Shaqiri anayepatikana kwa dau la Pauni 12 milioni tu kwa mujibu wa mkataba wake.

Pia, yupo kiungo wa Kibrazil anayetoa huduma yake pale Chelsea, Willian ambaye yuko tayari kuungana na Mourinho pale Old Trafford.

Halafu kuna kiungo fundi wa mpira, Sergej Milinkovic-Savic ambaye imeelezwa kuwa United wamekubali kuilipa Lazio Pauni 80 milioni ili kumleta Old Trafford. Viungo hawa wote wanafiti kubeba mikoba ya Pogba wakisambaza mipira kwa Neymar na Romelu Lukaku pale mbele.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s