Makala: Huyu ndio Firmino, nyota mwenye makali asiyepata “sifa stahiki” pale Anfield

Kuna neno zuri ambalo hubeba maana kubwa kwenye tasnia yoyote ama kwenye utendaji kazi wa taasisi yoyote ile, neno hilo linaitwa nyuma ya pazia. Nyuma ya pazia ni kule ambako hatukutazami kutokana na uwepo wa pazia ambalo huchukua “attention” yetu ama hukamata fikra zetu. Sifa ya mwanadamu ni kutazama kwa makini vile ving’aavyo kuliko vile visivyokuwa na mwanga.

01

Haya twende sawa.. kwenye tasnia ya habari sifa anapewa mtangazaji kuliko mzalishaji, kwenye tasnia ya uigizaji sifa za anayeigiza kuliko anayetayarisha na hata kwenye kilimo jembe hupata sifa kubwa kuliko mpini.

Ni bahati mbaya lakini hivi vyote lazima vitokee ili shughuli ikamilike, yule anayechafuka hasemwi kuliko aliyekuwa msafi na aliyekuwa nyuma hazungumzwi kama anayekuwa mbele akitazamika.

Turudi kwenye Soka

Kwenye soka haya ni maisha ya kawaida pia na maisha yaliyozoeleka kila kukicha. Katika dunia ya Cristiano Ronaldo huwezi kumzungumza Toni Kroos, dunia ya Lionel Messi huwezi kumtaja Andres Iniesta kwa heshima anayostahili na hata katika dunia ya Pogba na Lukaku ni wazi utashangaa De Gea anaonekana anatimiza wajibu wake.

Ni jambo la kawaida na lililozoeleka kwa sasa, hata mmea unaostawi huwa tunavutiwa kwa kiasi kikubwa na maua yake, matunda yake na muonekano wake kuliko kazi kubwa iliyofanywa na mizizi ama shina kuhakikisha kuwa mti ule unakuwa imara na upo mahala pake.

Tuingie kwa Salah kidogo

Salah

Huwezi kuizungumza dunia ya soka kwa sasa pasipo kumtaja Mohamed Salah, mshambuliaji hatari zaidi kwa sasa. Binadamu pekee ambaye kila anachokunywa kina ladha ya zabibu, kila anachoshika ni dhahabu na sauti yake akizungumza inakuwa na mvuto wa chombo cha muziki ambacho bado hakijagunduliwa duniani.

Yupo katika dunia ya kifikra ambayo watu wengi waliisubiri, dunia ambayo itaongezeka katika dunia mbili za Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Salah amefunga mabao mengi zaidi ya raia yoyote wa Afrika katika msimu mmoja wa klabu bingwa Ulaya, amefunga mabao mengi zaidi kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu ya England.

Ametwaa kila tuzo anayotaka kuipata kwa msimu huu wa ligi na mwaka 2018 haujawa mwaka wa Jeff Bezos kutangazwa kuwa tajiri namba moja duniani bali umekuwa wa Mohamed Salah kuwa mwanadamu anayejeruhi kila lango linalopita mbele yake, upo hapo!!

Amejenga urafiki na nyavu kuliko ngedere alivyokuwa na urafiki na miti, mabao yanafuata mkondo wa Mohamed Salah kuliko maji yanayotiririka mto msimbazi kwenda baharini. Hakuna mwanadamu anayefanya maajabu ambayo hayakutegemewa kama Mohamed Salah kwa sasa, amegusa kila nyoyo na ameipa faraja ndani ya Anfield na mpaka kuitwa mfalme kwao Misri.

Lakini huyu anabaki kuwa kioo cha televisheni na hakuna anayetazama uchogo uliojificha, anabaki kuwa eneo limulikalo mbele kwenye kurunzi na hakuna anayejali betri zimekaa wapi. Anayo makali ya upanga kukata kilichokuwa mbele yake na wakati mwingine kuwa shoka anapokutana na vitu vigumu zaidi lakini hakuna anayejali mpini upo wapi.

Anafanya madhara makubwa lakini kuna mwanaume ambaye ni muhimu zaidi ili nyumba anayoishi Mohamed Salah inayoitwa Liverpool iwe salama na inayokalika.

Huyu ndio Firmino

02

Huyu ndiye binadamu anayeamuru nguvu inayoweza kutumika siku hiyo kwenye kikosi cha Liverpool, anaamua kasi ya kukimbia ndani ya uwanja na anaamua kama iwe siku ya kivivu.

Yeye ndio jiko ambalo linatoa pishi la Liverpool linaloitwa “Geggenpressing” mfumo maarufu unaotumika na Liverpool katika kuizingira timu pinzani ili kupokonya mipira kwa haraka. Anaitwa Roberto Firmino, Mbrazil anayefanana na wenzake katika kupenda starehe lakini akitofautiana nao katika uchapakazi.

Kwenye macho ya Brendan Rodgers, Firmino alikuwa namba 10 ambaye asingeweza kutulia kwenye mfumo wake kwa sababu eneo hilo alitaka mbwembwe za akina Coutinho na Lallana zaidi.

Bahati mbaya matokeo mabaya ya Liverpool kwa wakati huo yakasababisha Firmino awe muhanga wa kutumiwa kwenye nafasi tofauti zaidi na kila mtu akaona hii ilikuwa hasara nyingine mpaka alipofika Jurgen Klopp.

Klopp alimweka katika nafasi ambayo binadamu wengi tunaotizama soka kupitia majukwaani na kwenye luninga tulimpinga kwa nguvu. Katika dunia wanayosajiliwa akina Lukaku, Morata unamweka vipi Firmino kama mshambuliaji wa kati?

Muda hausimami na majibu yapo mbele ya macho yetu na tunaona aibu kurejea kauli zetu ili tuzifute. Aibu zaidi ni kuwa bado huyu mtu haimbwi kwa sababu ni ngumu kuupima mchango wake kwa kutumia macho peke yake tofauti na Mohamed Salah.

Kwenye Ligi Kuu ya England, Roberto Firmino amekuwa mchezaji pekee kufanya “tackles” zaidi ya 60 na kutengeneza nafasi za kufunga zaidi ya 50.

Anafanya haya huku pia akiwa amefunga mabao kumi na tano na zaidi na akiwa ametoa pasi za mabao zaidi ya saba. Ni huyu huyu ambaye amefunga mabao 10 sawa na Mohamed Salah kwenye klabu bingwa Ulaya huku pia akiwa ametoa pasi za mabao saba, tatu zaidi ya Mohamed Salah.

Kwa lugha pana zaidi ni kuwa Roberto Firmino akiwa katika safu ya ushambuliaji kwenye ligi kuu ya England pekee ni nusu ya Mohamed Salah kwenye mabao, ni nusu ya Kevin De Bruyne kwenye kutoa pasi za mabao, ni nusu ya Wilfred Ndidi na Ng’olo Kante kwenye kukaba na nusu ya Mesut Ozil kwenye kutengeneza nafasi za kufunga.

Tafsiri kamili ni kuwa kwenye mwili wa Roberto Firmino kuna nusu ya Salah, Nusu ua De Bruyne, nusu ya Kante na nusu ya Ozil kwa pamoja. Unataka nini zaidi?

Hii ndio sababu kwanini Jurgen Klopp aliwahi kuona kitu ambacho wengi hatuoni, ndio sababu kipenzi cha kwanza Klopp sio kipenzi cha kwanza cha watazamaji.

Kwenye mfumo wa Klopp, hakuwezi kuwepo kwa Liverpool inayocheza uwanjani bila Firmino, kwenye macho ya Klopp hakuna mfumo wa Liverpool bila mtu huyu na kwenye Oblongata yake Klopp hakuna balaa la ushambuliaji la Liverpool bila Firmino.

Firmino anabaki kuwa mpini unaoshikilia makali ya Liverpool, mpini ambao ndio ushikwa na kuelekeza makali yafanya lipi na kwa nguvu ipi. Lakini bahati mbaya anakuwa nyuma, nyuma kama betri zinapotoa chaji ili kurunzi (tochi) iweze kuwaka. Anafanya kazi kubwa ambayo ni ngumu kuigundua kupitia mboni za macho peke yake.

Mane alikuwa mchezaji bora msimu uliopita kwa sababu ya Firmino, Salah amekuwa hatari kuliko ilivyotegemewa kwa sababu ya Firmino na anaweza kuja mwingine akafanya makubwa kwa sababu yake huyu. Aina yake ya uchezaji inawapa nafasi kubwa wachezaji wengine kufanya mambo ya msingi tu huku barabara ngumu zote akipitia yeye. Hapewi heshima yake.

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s